Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan leo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa Masoko ambayo inatarajiwa kutengeneza ajira kwa Watanzania takribani 30,000 huku katika hatua za awali za ujenzi, ajira za muda mfupi 278 zimetolewa ambapo kati ya hizo ajira 106 sawa na 38% zimetolewa kwa Wakazi wa Wilaya za Mkoa wa Lindi.
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe hilo la msingi la ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa akiwa Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika Mikoa ya Mtwara na Lindi, Wizara ya Uvuvi imesema bandari ya aina hiyo haijawahi kuwepo tangu Nchi ya Tanzania ipate uhuru
Kukamilika kwa bandari hiyo kutawezesha meli za uvuvi zinazovua katika ukanda wa uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari Kuu kutia nanga na kushusha samaki wanaolengwa na wale wasiolengwa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya Nchi.
Pia, uwepo wa bandari ya uvuvi utachochea uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi, hivyo uwekezaji huu, unaenda kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya Nchi kutoka tani 40,721.53 zenye thamani ya USD milioni 249.54 hadi tani 52,937.99 na kuchangia takriban asilimia 10 katika pato la Taifa ifikapo mwaka 2036.
Pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya uvuvi, Rais Samia pia amegawa boti 34 kati ya boti 160 ambazo zinatolewa Nchi nzima, boti hizi kwa ukanda wa Bahari ya Hindi zipo 92 zikihusisha Wavuvi na Wakulima wa mwani.