Bandari za ziwa Victoria zimeweza kuvuka lengo la kuhudumia shehena ya mzigo mbalimbali kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 kutoka kwenye lengo lililowekwa jambo ambalo limeelezwa kuwa, limetokana na serikali kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika kutekeleza miradi ya maboresho katika bandari hizo.
Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 bandari za ziwa Victoria ziliwekewa lengo la kuhudumia shehena tani 228,000 ambapo hadi kufikia mwezi Mei, mwaka huu jumla ya tani 246,000 zimeshahudumiwa (sawa na ufanisi wa asilimia 101.1) na kwa muda uliobaki upo uwezekano wa kuongezeka zaidi kiwango cha shehena.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Mei 31, 2023 na Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Ferdinand Nyathi akiongea na waandishi wa habari ambapo amesisitiza kuwa, bandari hizo zimefanya vizuri katika maeneo yote ikiwemo mapato, kuhudumia shehena pamoja na idadi ya meli zinazoingia katika bandari hizo.
Nyathi ameongeza kuwa, miradi yote ya maboresho katika bandari za Ziwa Victoria inalenga kuboresha maeneo yote ya bandari hizo ikiwemo kuongeza kina cha maji, kuboresha maegesho ya meli, kuhudumia meli kubwa, miundombinu ya reli zinazoingia bandarini, majengo ya abiria, maeneo ya kuhifadhia mizigo, mifumo ya TEHAMA pamoja na mifumo ya ulinzi na usalama.
Kufuatia hilo, Nyathi ametoa wito kwa jumuiya ya wafanyabiashara kuendelea kutumia bandari za ziwa Victoria kwani huduma zao ni nzuri na zimeboreshwa huku wakitoa kipaumbele cha kuwasikiliza wafanyabiashara hao.
“Niwaombe jumuiya ya wafanyabiashara tuendelee kutumia bandari zetu za ziwa Victoria kwani huduma ni nzuri na tunawasikiliza kwa kutumia njia sahihi ya kuwa wasikivu na kuhudumia mizigo yao kwa ufanisi ili kuhakikisha kwamba malengo yao kibiashara yanatimia” alisema Nyathi
Vilevile ameeleza kuwa, kwa sasa bandari hizo zinahudumia shehena ya mizigo inayokwenda katika bandari ya Kisumu jambo ambalo halikuwepo katika miaka miwili iliyopita.
“Kama miaka miwili iliyopita tulikuwa hatupati mizigo inayokwenda katika bandari ya Kisumu, lakini kuanzia mwaka huu wa fedha tumeanza kupata mizigo ya kwenda katika bandari hiyo” alisisitiza Nyathi na kuongeza
“Mzigo inayotoka na kwenda nchi jirani inachangia asilimia 50 ya mizigo yote inayohudumiwa katika bandari zetu za ziwa Victoria”
Kwa upande wa miradi inayotekelezwa hivi sasa, meneja huyo amesema
“Nipongeza serikali kiasi ambacho kimetengewa kwaajili ya kuendeleza bandari zetu za ziwa Victoria ni kikubwa sana. Kuna miradi tayari imeshaanza kutekelezwa katika bandari za Bukoba na Kemondo ikiwa thamani ya takribani shilingi bilioni 40”
Wakiongea kwa nyakati tofauti, mawakala wa Forodha Peter Zakayo na Simon Digomba wamesema, ushirikiano wa kutosha wanaupata kutoka viongozi na watumishi wa bandari za ziwa Victoria na huduma zinazotolewa na bandari hizo ni nzuri ikiwemo kutolewa mizigo kwa wakati.
Naye Mhandisi wa Meli kutoka Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) amesema, kupitia maboresho yanayofanyika ni zao la mawasiliano kufuatia uwekezaji mkubwa wa ujenzi meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu ambayo itatumika katika shughuli za usafiri na usafirishaji katika bandari za ziwa Victoria ambayo mahitaji yake yamekidhiwa na miradi ya maboresho katika bandari bandari hizo.
Ziwa Victoria lina bandari nyingi lakini zilizo kubwa ni Mwanza Kusini na Mwanza Kaskazini ambazo zinaungwa na barabara na reli nchini na nchi jirani. Bandari hizi zina miundombinu ya kutosha, kuwezesha huduma za bandari ikiwamo mizani ya magari, matangi ya mafuta, karakana na jengo la abiria.Mbali na bandari hizi mbili Ziwa Victoria lina bandari nyingi zinazofanyakazi ya kutoa huduma kwa umma