Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha limemuomba Waziri wa Maliasili na Utalii Dk.Hamis Kigwangala kusitisha operesheni ya kuwaondoa wananchi wa vijiji 15 wanaoishi ndani ya eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Emmanuel Shangai amelisoma tamko hilo,katika kikao cha baraza la madiwani na baadaye baraza hilo liliridhia kama azimio la pamoja na kupinga operesheni hiyo.
Akisoma tamko hilo, alisema wananchi wa vijiji 15 ndani ya Mamlaka hiyo, imependekezwa waondolewe kupisha uhifadhi jambo ambalo linakiuka sheria ya kuanzishwa Mamlaka hiyo na pia sheria za nchi.
“Lakini pia wananchi ambao wanaishi maeneo ya nyanda za juu wanatakiwa kuondolewa na kuhamishiwa nyanda za chini katika maeneo ambayo hayafai kwa makazi na ufugaji kutokana na kuathiriwa na uvamizi wa maguguna hakuna maji na malisho”
Shangai aliomba baraza hilo kupitisha azimio kuitaka Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro,kusitisha operesheni na kuacha kuwanyanyasa wananchi ambao ni wenyeji katika eneo hilo lakini pia Waziri wa Maliasili na Utalii, kusitisha zoezi hilo kwani pia halishirikishi wananchi na serikali za vijiji.
Baada ya tamko hilo madwani walichangia mjadala na kuunga mkono kusitishwa operation hiyolakini pia wakitaka wananchi wanaoishi ndani ya eneo hilo washirikishwe sambamba na viongozi wa serikali ngazi za vijiji na Kata.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Methew Siloma alisema ni muhimu kusitishwa operesheni hiyo lakini pia watu wanaotuhumiwa kunyanyasa wananchi ndani ya Mamlaka hiyo, wachukuliwe hatua za kisheria.
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Rashidi Taka alisema serikali haitakubaliana na mpango wowote wa kunyanyasa wananchi katika wilaya hiyo na kuwahakikishia kamati iliyoundwa kushughulia suala la ardhi mseto Ngorongoro inapaswa kuwashirikisha wananchi.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha uhifadhi unaendelea ngorongoro lakini pia kujali maendeleo ya wananchi wanaoishi ndani ya Mamlaka hiyo.
“kama kuna changamoto tutafatilia na kuzipeleka ngazi husika ili kuhakikisha mpango wa ardhi mseto unakuwa shirikishi”
Mwaka 2019 Waziri Dk.Kigwangala aliunda kamati ya kufanya tathmini ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro iliyokuwa na lengo la kuboresha uhifadhi, kutatua migogoro na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi ndani ya eneo hilo.
VIDEO: SEHEMU YA MAZOEZI YA MAFUNZO YA KIJESHI, WAKILA KIAPO MBELE YA MKUU WA MAJESHI MABEYO