Baraza la Mawaziri la nchini Zimbabwe limevunjwa jana jumatatu baada ya kufanya kikao chake cha mwisho kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika kesho jumatano.
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amewapongeza wajumbe wa Baraza hilo kwa umoja wao na kazi ngumu walizofanya katika kipindi cha miaka mitano, akisema ameona serikali ya chama cha ZANU-PF ikitekeleza majukumu yake na kupata matokeo halisi katika nyanja ya uchumi na jamii.
Kesho jumatano, Wazimbabwe watapiga kura katika uchaguzi mkuu na kuchagua rais, wabunge, na wawakilishi wa serikali za mitaa.
Rais Mnangagwa anagombea wadhifa huo kwa muhula wa pili, na mshindani wake mkuu ni Nelson Chamisa, kiongozi wa chama cha upinzani cha Muungano wa Wananchi kwa Mabadiliko (CCC).