Mlinda mlango wa Poland Wojciech Szczesny ameachana na taarifa za kustaafu baada ya kusajiliwa na miamba ya Uhispania Barcelona Jumatano.
“Barcelona na mchezaji Wojciech Szczesny wamefikia makubaliano ya kusainiwa kwake hadi Juni 30, 2025,” walisema viongozi hao wa La Liga katika taarifa.
Kipa huyo wa zamani wa Arsenal na Juventus, 34, anajiunga baada ya mlinda mlango chaguo la kwanza wa Barca Marc-Andre ter Stegen kutoshirikishwa hadi mwisho wa msimu huu kutokana na jeraha baya la goti alilopata Septemba 22.
Szczesny alistaafu msimu huu wa joto baada ya kushiriki Euro 2024 akiwa na Poland lakini sasa amerejea kwenye mchezo huo kucheza La Liga kwa mara ya kwanza.
Kipa huyo alisema “moyo wake (haukuwa) huko tena” kucheza kandanda baada ya kuondoka Juventus kwa makubaliano ya pande zote mwezi Agosti.
Szczesny amecheza zaidi ya mechi 600 kwa klabu na nchi katika maisha yake ya soka, akishinda mataji matatu ya Serie A na makombe matatu ya Italia akiwa na Juventus, pamoja na Vikombe viwili vya FA akiwa na Arsenal.