Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, ameuagiza Wakala wa Majengo (TBA) kuhakikisha unakusanya deni la Shilingi Bilioni 81.5 wanazodai kwa wapangaji wao sambamba na kuwaondoa wadaiwa sugu katika nyumba hizo ili upatikanaji wa fedha hizo uweze kusaidia utekelezaji wa miradi mingine nchini.
“TBA simamieni sheria kwa yeyote asiyelipa kodi hata kama ni kiongozi, waandikieni notisi ya kulipa madeni yao na wasipolipa waondoeeni, wapo wengine nje wanasubiri wapewe nyumba ili waweze kulipa kodi kwa wakati na tutamia makusanya hayo kujenga nyumba nyingine”, amesisitiza Bashungwa.
Ameyasema hayo leo Septemba 07, 2023 jijini Dodoma wakati Waziri huyo alipofanya ziara yake kwa mara ya kwanza katika Wakala huo na kuzungumza na menejimenti ya TBA ambapo amesisitiza uwekezaji wenye tija kwa watumishi na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Bashungwa ameagiza TBA kuhakikisha wanakuja na mikakati itakayosaidia kujenga nyumba za bei nafuu hasa kwa vijana wanaoajiriwa katika utumishi wa umma hususan Dodoma ili kuweza kumudu gharama za maisha.
“Kuna vijana ambao wanaingia kwenye kada ya utumishi wa umma na bado hawajawa na uwezo wa kujijengea nyumba, kupitia TBA mnaweza kujenga nyumba za bei rahisi kwa ajili ya vijana hao ili kuwarahisishia gharama za Maisha”, amesema Bashungwa.
Kadhalika, Bashungwa ameutaka Wakala huo kuwa na utaratibu wa kuwajengea uwezo wataalamu walionao ili kuenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia hasa katika suala la ujenzi na uendelezaji wa majengo mbalimbali.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, amesema kuwa Wakala huo utahakikisha unatafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo na kumuahidi Waziri Bashungwa kuandaa mikakati mizuri itakayosaidia Wakala huo kutoa huduma bora kwa wananchi.
Awali, Arch. Kondoro ameeleza kuwa hadi sasa TBA inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 za watumishi wa umma eneo la Nzuguni Dodoma ambapo awamu ya kwanza ya nyumba 150 utekelezaji umefikia asilimia 95 na awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 150 utekelezaji wake umefikia asilimia 10.
Miradi mingine ni ujenzi wa nyumba 20 za Viongozi jijini Dodoma ambazo zililenga kukabiliana na uhaba wa nyumba za Viongozi baada ya Serikali kuhamia Dodoma ambapo mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na nyumba zimeanza kutumiwa na Viongozi.
Waziri Bashungwa anaendelea na ziara yake ya kutemebelea Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi ambapo leo ametembelea na kuzungumza na menejimenti ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).