Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amekabidhiwa ofisi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ambaye Sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), leo tarehe 13 Disemba, 2024 jijini Dodoma.
Makabidhiano hayo yamefanyika ikiwa ni siku nne baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwaapisha Mawaziri hao tarehe 9, Disemba 2024, Tunguu Zanzibar.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Waziri Bashungwa amemshukuru mtangulizi wake kwa makabidhiano ambayo yatakuwa mwongozo wa kusimamia na kutekeleza majukumu yaliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani Nchi.
Sambamba na hilo, Waziri Bashungwa ameshukuru Rais. Dkt Samia ambapo amesema kuwa “Niendelee kumshukuru Rais wetu na nimuahakikishie kama ambavyo alituelekeza wakati anatuapisha kwamba niendeleze pale ulipoishia Waziri Masauni”.
Aidha, Bashungwa amesisitiza suala la Watumishi wa Wizara na vyombo vyake vya usalama kufanya kazi kwa kushirikiana ili kwa pamoja kusimamia na kutekekeleza majukumu yao kikamilifu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamadi Masauni amemueleza kuwa Waziri Bashungwa anaipokea Wizara ikiwa katika hali nzuri na hali hiyo inatokana na namna Mheshimiwa Rais Samia alivyoiwezesha kibajeti Wizara hiyo.
“Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana miongoni mwa kazi aliyoifanya ni kuiwezesha Wizara kuwa na uwezo wa kutekeleza zaidi majukumu yake.” amesema Waziri Masauni.
Waziri Masauni ameeleza kuwa Wizara inaendelea na utekelezaji wa maelezeko ya Tume ya Haki Jinai ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Wananchi wanahudumiwa kwa haki, bila uonevu wala dhuluma.
Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Maduhu Kazi.