Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameshiriki Misa Takatifu katika Parokia ya Mtakatifu Paulo na kuongoza harambee ya kumalizia ujenzi wa jengo la ofisi za Jimbo Katoliki la Bunda ambapo jumla ya Shilingi Milioni 272.6 imekusanywa.
Harambee hiyo imefanyika leo Novemba 10, 2024 Wilayani Bunda Mkoani Mara ambapo pamoja na mambo mengine, Waziri Bashungwa amezindua ofisi ya Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda, Mhashamu Simon Chibuga Msondole ambayo itaanza kutoa huduma za kijamii na kiroho.
“Jimbo letu la Bunda ni changa lina miaka 13, tunahitaji kubadilisha sura ya Jimbo letu, ili itakapofika Jubilei ya miaka 25, Jimbo liwe limepiga hatua kubwa na lenye kupendeza, lenye miundombinu mbalimbali kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu na nchi yetu”, amesema Bashungwa
Bashungwa amelishukuru Kanisa Katoliki nchini kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika shughuli za ustawi na maendeleo ya jamii katika Sekta ya Elimu, Afya, na Sekta za uzalishaji hususani kilimo, uwekezaji katika viwanda, Hoteli pamoja na bima za aina mbalimbali.
Aidha, Bashungwa amemshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara, madaraja, mizani, vivuko na Kiwanja cha Ndege katika Mkoa wa Mara ambapo amebainisha baadhi ya miradi iliyokamilika, inayoendelea kutekelezwa na ambayo ipo katika hatua za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Akitaja miradi hiyo, Amesema ujenzi wa barabara ya Nyamuswa – Bulamba (km 56.4) umekamilika kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Shilingi Bilioni 67.8 na kukamilika kwa ujenzi mzani wa kupima magari yakiwa kwenye mwendo (Weigh in Motion) katika eneo la Rubana kwa Shilingi Bilioni 22.2
Bashungwa amebainisha miradi mingine ni ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Sanzate – Nata (km 40) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 51.08 ambao umefikia asilimia 55, ujenzi wa barabara ya Mogabiri – Nyamongo (km 25) kwa gharama ya shilingi Bilioni 34.6 na ujenzi umefikia asilimia 52.
Kadhalika, Bashungwa ameongeza kuwa Serikali inaendelea na ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Musoma kwa Shilingi Bilioni 35.048 na utekelezaji wake umefikia asilimia 57.
Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda, Mhashamu Simon Chibuga Msondole amewashukuru viongozi wote wa Serikali, vyama vya kitume, waumini wa Parokia hiyo, marafiki na jamaa kwa majitoleo yao katika kufanikisha ujenzi wa ofisi za Parokia ya Bunda.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Chacha Maboto ametoa rai kwa uongozi wa Jimbo Katoliki la Bunda kuhakikisha wanasimamia kikamilifu michango yote iliyotolewa katika harambee hiyo ili ziweze kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Akisoma Risala, Mwenyekiti wa Kamati ya Harambee Jimbo la Bunda, Kulwa Kahabi amesema kuwa harambee hiyo imehusisha waumini wa Parokia 23, vyama vya kitume, watu binafsi na kufafanua harambee hiyo imekusanywa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza mwaka 2022 na walikusanya Milioni 240, awamu ya pili mwaka 2023 walikusanya Milioni 130 na katika mwaka 2024 matarajio yao ni kukusanya Milioni 350.