Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kwa kujenga miundombinu ikiwemo Masoko ili kurahisisha ufanyaji wa biashara.
Bashungwa ameeleza hayo Mkoani Pwani leo Oktoba 09, 2024 wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua Soko la Kisasa la Bwilingu pamoja na miundombinu yake lillilopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze lililogharimu Shilingi Bilioni 1.7.
Bashungwa ameeleza kuwa Serikali imejenga Soko hilo kwa kutambua Chalinze ipo kwenye eneo la kimkakati linalounganishwa na reli ya kisasa (SGR) na kuunganisha Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Dodoma.
“Bilioni 1.7 zilielekezwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia zitolewe katika Halmashauri ya Chalinze katika mapato yake ya ndani wanayokusanya ili zifanikishe ujenzi wa Soko hili la kisasa“, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze pamoja na Waheshimiwa Madiwani kwa kusimamia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwa mfano wa kuigwa kwa Halmashauri zingine kutumia fedha za ndani wanazokusanya kuboresha na kufikisha huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi.
Aidha, Bashungwa amewaagiza watalaam kutoka Idara ya Masoko na Biashara katika Halmashauri hiyo kuhakikisha wanawatembelea mara kwa mara wafanyabiashara katika Soko hilo na kutoa elimu ya biashara ili kusaidia kukuza mitaji ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa.
Bashungwa ameeleza kuwa kukamilika kwa Soko hilo kutaondoa adha waliyokuwa wanaipata wafanyabiashara wa Halmashauri ya Chalinze kwa kukosa mahala salama pa kufanyia biashara.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameeleza kuwa ujenzi wa Soko hilo ni mkakati ws kuhakikisha Halmashauri inakuwa na sehemu bora na yenye mpangilio kwa kutoa huduma kwa wananchi pamoja na kuongeza vyanzo vya mapato.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wananchi wa Halmshauri ya Wilaya ya Chalinze wamemshukuru Rais Samia kwa kuelekeza fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Soko hilo ambalo limewarahisishia kufanya biashara na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.