Mkurugenzi Mtendaji wa Bayer Leverkusen, Fernando Carro amesema ana imani klabu hiyo inaweza kudumisha mafanikio yao iwapo Xabi Alonso ataondoka msimu wa joto, na kuongeza kuwa sio “kila kitu kitaharibika wakati hayupo.”
Leverkusen wako tayari kuvunja ukiritimba wa miaka 11 wa Bayern Munich juu ya taji la Bundesliga msimu huu chini ya usimamizi wa Alonso. Ushindi wa 3-0 dhidi ya Wolfsburg siku ya Jumapili ulikuwa ushindi wao wa 21 msimu huu na kuwafanya wadumishe uongozi wao wa pointi 10 kileleni mwa jedwali.
Vinara hao wa ligi hawajafungwa katika michezo 36 katika mashindano yote msimu huu. Leverkusen wana safu bora ya ulinzi kwenye Bundesliga wakiwa wameruhusu mabao 16 pekee katika mechi 25, huku Bayern pekee ndiyo waliofunga zaidi.
Mafanikio hayo yamemfanya Alonso kuwa mmoja wa makocha wanaotafutwa sana barani Ulaya, ripoti zikimuhusisha nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Uhispania na Liverpool na Bayern haswa.
Carro, hata hivyo, alisema Leverkusen wamejiandaa vyema iwapo Alonso atahama kutoka klabu hiyo.
“Tunafurahi kuwa yuko hapa, lakini Xabi Alonso ni kipande cha puzzle. Sio kama kila kitu kitaanguka wakati hayupo,” Carro alisema katika mahojiano na DAZN.
“Tuna kikosi cha juu, tuna wafanyakazi wa kufundisha, [mkurugenzi wa michezo] Simon Rolfes … Kwa hiyo, watu wengi wanaohusika na mafanikio wako hapa, bila ya Xabi Alonso.”