Benjamin Mendy amewasilisha madai ya mamilioni ya pauni dhidi ya klabu yake ya zamani ya Manchester City kuhusu mishahara ambayo haijalipwa, wakili wake alithibitisha kwenye kituo cha habari cha ESPN.
Mendy, 29, aliachiliwa kwa kosa moja la ubakaji na lingine la kujaribu kubaka katika kesi iliyosikilizwa tena mwezi Julai, kufuatia hukumu ya kutokuwa na hatia aliyopokea kwa makosa sita ya ubakaji na shtaka moja la unyanyasaji wa kingono mwezi Januari.
Mashtaka dhidi ya Mendy yaliifanya Man City kumsimamisha kazi beki huyo mwezi Agosti, 2021 kabla ya hatimaye kusitisha malipo yake Septemba, 2021. Beki huyo alisaini Lorient ya Ligue 1 kwa uhamisho wa bure msimu huu wa joto baada ya kumalizika kwa mkataba wake City.
Nick De Marco KC, ambaye anasimamia kesi kwa niaba ya Mendy, aliithibitishia ESPN kwamba mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa amewasilisha madai ya pauni milioni kadhaa kwa kukatwa kwa mishahara bila kibali kwenye Mahakama ya Ajira.
“Manchester City FC ilishindwa kumlipa Bw Mendy ujira wowote kuanzia Septemba 2021, kufuatia Bw Mendy kushtakiwa kwa makosa mbalimbali ambayo yote aliachiliwa huru, hadi mwisho wa mkataba wake Juni 2023. Madai hayo yatawasilishwa mbele ya mahakama Mahakama ya Ajira,” alisema katika taarifa iliyotumwa kwa barua pepe kwa Reuters.
Mendy, ambaye alisajiliwa na City kutoka Monaco mwaka 2017, aliichezea klabu hiyo ya Ligi Kuu mara 75 na kushinda mataji matatu katika muda wake huko. Mechi yake ya mwisho akiwa na City ilikuwa dhidi ya Tottenham Hotspur mnamo Agosti, 2021.