Benjamin Netanyahu amesema atajadili “ushindi dhidi ya Hamas”, Iran na kupanua uhusiano wa kidiplomasia na nchi za Kiarabu katika mkutano wake na Donald Trump.
Mkutano huo utakaofanyika Ikulu ya Marekani Jumanne utakuwa wa kwanza kwa Bw Trump kuwa na kiongozi wa kigeni tangu arejee afisini.
Inakuja wakati wapatanishi wa Marekani na Waarabu wakianza kuratibu awamu inayofuata ya makubaliano ya kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza na kuwaachilia makumi ya mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo.
Katika taarifa iliyotolewa kabla ya kuondoka kwake kuelekea Washington, Waziri Mkuu wa Israel alisema watu hao wawili watajadili “ushindi dhidi ya Hamas, kufanikisha kuachiliwa kwa mateka wetu wote, na kukabiliana na mhimili wa ugaidi wa Iran katika vipengele vyake vyote”.
Alisema kwa kufanya kazi pamoja, wanaweza “kuimarisha usalama, kupanua mzunguko wa amani na kufikia enzi ya ajabu ya amani kupitia nguvu”.
Kundi la Hamas ambalo limethibitisha kwa haraka tena udhibiti wake wa Gaza tangu usitishaji mapigano ulipoanza mwezi uliopita, limesema halitawaachilia mateka hao kutokana na kuwa huru katika awamu ya pili bila kumalizika kwa vita na kuondoka kikamilifu kwa majeshi ya Israel.