Katibu wa NEC – Oganaizesheni wa CCM Taifa, Ndg. Issa Haji Gavu, amesema serikali iliyopo madarakani inayotokana na CCM katika kuendeleza utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini imejipanga kuboresha stendi ya mabasi mkoani Geita ili wananchi waondokane na usumbufu wanaopata wakati wa kwenda kupata huduma ya usafiri.
Akieleza kwa undani zaidi, Ndg. Gavu amesema tayari serikali inayongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetenga kiasi cha Tsh 14 na utaratibu wa kumpata mkandarasi upo tayari hivyo mradi huo kuanza kutekelezwa hivi karibuni.
Ndg. Gavu ameyasema hayo tarehe 20 Novemba, 2024 katika ufunguzi wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 mkoani Geita akiwa ndiye mgeni rasmi.
Pia, Ndg. Gavu ameeleza kuwa yapo maeneo mbalimbali katika mji wa Geita ambayo yalikuwa hayajaimarika katika miundombinu ya barabara za lami hivyo serikali ya CCM imetenga fedha na kuanza mradi wa ujenzi wa Km 17 za kiwango cha lami katika mji wa Geita ikiwa lengo ni kuimarisha mawasiliano na kupandisha hadhi mji wa Geita.
Aidha, Ndg. Gavu amesema ndani ya Geita zimejengwa shule 180 mpya zikiwemo za msingi na sekondari ambapo ndani yake ipo shule maalum ya wasichana yenye thamani ya Tsh bilioni 3 ili kuonesha serikali ya CCM inamjali mtoto wa kike katika umuhimu wa kupata elimu.
Akizungumza katika kuendelea kuwaomba wananchi kura, Ndg. Gavu amesema _ni imani ya CCM ya kuwa wananchi wa Geita maeneo mengine nchini wataendelea kukimanini Chama Cha Mapinduzi kwakuwa kimendelea kuonesha uchapakazi wake wenye dhamira ya kuendelea kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya watanzania._
Vilevile, Ndg. Gavu amewasihi wananchi kuendelea kuitunza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo imekuwa ikitekelezwa na serikali kwakuwa itaendelea kutupa huduma kubwa na muhimu kwa jamii yetu.
Akizungumza sekta ya Afya, Ndg. Gavu ameeleza kuwa ndani ya Geita imejengwa hospitali kubwa yenye thamani ya Tsh bilioni 20 kuimarisha huduma za afya kwa wananchi._