Mfanyabiashara maarufu wa Marekani, Elon Musk amekuwa Mtu wa kwanza katika historia duniani kufikisha thamani ya juu ya utajiri wa dola bilioni 400 za Kimarekani (sawa na trilioni 972,240,000,000,000/- za Kitanzania) baada ya kuongezeka kwa utajiri wake kutokana na ushindi wa Rais mteule Donald Trump katika uchaguzi wa Marekani uliofanyika Novemba mwaka huu.
Ripoti zinaeleza kuwa Utajiri wa Musk kwa sasa ni mara mbili ya Mtu tajiri wa pili duniani ambaye ni Jeff Bezos mwenye utajiri unakadiriwa kufikia dola bilioni 244 za Kimarekani (sawa na trilioni 593,066,400,000,000/- za Kitanzania), Kwa mujibu wa Bloomberg utajiri wa Musk umeongezeka kutokana na kupanda kwa hisa za Kampuni yake ya Tesla na SpaceX.
Hisa za Tesla zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 tangu wakati wa uchaguzi wa Marekani huku kukiwa na matarajio kwamba Rais mteule, Donald Trump atafutilia mbali kanuni zinazoonekana kurudisha nyuma maslahi ya biashara za Musk na kumfanya aendelee kufanya vizuri zaidi kutokana na nafasi aliyopewa ya kusimamia Ufanisi wa Serikali ya Trump atakapoanza kazi mwezi Januari mwakani.