SERIKALI imefafanua kuwa imeweka tozo ya Sh900 katika kila lita ya mafuta ya petroli ili kufanikisha ukarabati wa barabara, kuboresha huduma za maji, elimu na nishati hasa kwa maeneo ya vijijini.
Waziri wa Nishati Januari Makamba ameliambia Bunge wakati akiwasilisha taarifa ya serikali kuhusu hali ya mafuta nchini ambapo serikali imetangaza ruzuku ya Sh bilioni 100 ili kupunguza bei ya mafuta nchini.
Kwa mujibu wa Makamba, tozo hiyo ambayo mchanganuo wake haukuwekwa wazi mara moja imekuwa ikisaidia katika ujenzi wa reli, ukarabati wa barabara za kitaifa na kugharamia elimu bila malipo.
Hata hivyo Makamba amesema ingawa serikali hutoza kiasi hicho cha pesa, bado gharama ya mafuta nchini iko chini ukilinganisha na nchi zingine zinazotegemea mafuta kutoka nchi za nje.
“Tuliamua kuweka tozo hii ili kuharakisha maendeleo vijijini,” amesema Makamba Bungeni jijini Dodoma.
Mwaka jana, serikali ilipunguza tozo za taasisi za serikali na kwa sasa ni Sh 38 kwa lita. Waziri Makamba ameonya kuwa punguzo zaidi kwa tozo hizo haliwezi kuleta nafuu katika bei ya mafuta ambayo asilimia 56 inategemea soko la dunia na asilimia 20 ikiwa ni gharama ya usafirishaji.
Serikali ilisema inakamilisha mazungumzo kupata mkopo wa masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha la Dunia and Benki ya Dunia ili kupata ahuweni ya kupanda kwa bei ya mafuta katika mwaka ujao wa fedha.