Tume ya Uchaguzi ya Liberia imemtangaza Joseph Boakai kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais na kumshinda rais wa sasa wa nchi hiyo, George Weah.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Bw. Davidetta Browne Lansanah amewaambia waandishi wa habari jana baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu kura, Boakai alipata asilimia 50.64 ya kura, na Weah alipata asilimia 49.36 ya kura.
Joseph Boakai, mgombea wa upinzani mwenye umri wa miaka 78 ambaye anaelezea umri kama “baraka”, amepongezwa na kiongozi aliyeko madarakani baada ya uchaguzi wa rais uliokuwa na ushindani mkubwa nchini Liberia.
Matokeo ya hivi punde yanampa ushindi wa pekee dhidi ya nyota wa zamani wa kandanda George Weah katika kinyang’anyiro kikali zaidi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 2017, Boakai hakuchoka, badala yake aliazimia kujaribu tena bahati yake.
Katika duru ya kwanza ya uchaguzi huu, si Boakai wala Weah aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zinazohitajika ili kupata ushindi, hivyo wakakabiliana katika duru ya pili ya uchaguzi.
Boakai anaelezea safari yake ya kuwa rais kwa muda mrefu, lakini anasema kwamba amedhamiria kusaidia “mamilioni ya Waliberia ambao wameachwa kukabili umaskini, magonjwa, na ukosefu wa usalama”.