Watumiaji wa maji ya mto Morogoro wapo hatarini kupata magonjwa ya mlipuko ikiwemo kupindupindu kutokana na baadhi ya watu kutupa uchafu nyakati za usiku katika mto huku baadhi yao wakifanya makazi katika baadhi ya madaraja yaliyopo katika mto huo na kujisaidia ndani ya mto.
Ayo TV imeshuhudia vijana zaidi ya sita wakiwa wamelala kwenye moja ya daraja lililopo katika mto huo eneo la Nunge Manispaa ya Morogoro huku wakikiri kujisaidia ndani ya mto.
Mmoja wa vijana waliokutwa wamelala ndani ya daraja Yasini Juma anasema nyakati za usiku wamekuwa wakishuhudia Watu walitupa takataka katika mto huo kisha kukimbia jambo ambalo limekua changamoto katika eneo hilo.
Kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu imeanza oparesheni ya kusafisha mito iliyopo mkoani Morogoro pamoja na kuwaondoa watu walioweka makazi ya kudumu katika maeneo ya madaraja na kusababisha uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji na kuhatarisha usalama wa madaraja hayo.
Katika oparesheni hiyo baadhi ya vijana wanaotumia madawa ya kulevya wamekiutwa wakiwa wameweka makazi ya kudumu chini ya daraja la mto Morogoro ,ambapo vijana hao wameeleza sababu ya kuweka makazi katika eneo hilo ni kukosa sehemu za kuishi hali inayochangiwa na ugumu wa maisha.
Meneja wa rasilimali za maji Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu Martin Kasambala amesema zoezi hilo litakuwa ni endelevu katika maeneo yote ya vyanzo vya maji na vijana watakaokutwa katika maeneo ya vyanzo vya maji watapatiwa elimu pamoja na kutafutiwa shughuli mbadala.
Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu wamekua wakiendesha zoezi la usafi kwenye maeneo yote ambayo yapo chini ya bodi hiyo kwa usimamizi huku msisitizo ukitolewa kwa wananchi kufuata sheria za utunzaji mazingira kwenye vyanzo vya maji.