Wafugaji wilayani Pangani Mkoani Tanga wametakiwa kuacha kufuga kimazoea na kuanza kufuga kisasa ili kuwezesha mifugo yao kukidhi mahitaji ya nyama bora kwenye masoko ya nje ya nchi.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Mifugo wa Bodi ya Nyama Kanda ya Kaskazini, KEFA MANASE wakati akitoa elimu juu ya unenepeshaji na ufugaji wa kisasa kwa wafugaji katika kata ya Mikinguni wilayani Pangani kwa wafugaji zaidi ya 60.
Akizungumza na millardayo.com wakati wa mafunzo hayo, Manase amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa elimu wafugaji kuondokana na ufugaji wa mazoea wa kufuga mifugo mingi na badala yake wafuge kisasa ili kuweza kupata faida na mifugo yao kuwa na nyama bora ambayo itakidhi vigezo vya masoko kimataifa.
“Kufanya unenepeshaji kwa mfugaji ina faida kubwa kwa mfano mfugaji anapofanya unenepeshaji ni rahisi mifugo kufikia uzito unaohitajika sokoni kwa haraka lakini kwa upande mwingine mfugaji anaweza kuvuna mifugo mingi kwa wakati mmoja jambo ambalo litampa faida kubwa zaidi.
“Lakini pia, unenepeshaji unaongeza ubora wa nyama, hivyo sisi kama taasisi tumekuwa tukijitahidi kuwaelimisha wafugaji ili wafikie mahitaji ya soko ambayo tunayatafuta nje ya nchini,” amesema.
Aidha, amesema kanuni za ufugaji bora ambazo wafugaji wanatakiwa kuzifuata ambazo ni kuvuna mifugo yao kwa wakati, kutumia mbegu ambazo zimeboreshwa, kwani faida za kutumia mbegu zilizoboreshwa yaani chotara ni rahisi kufikia uzito wa soko haraka.
“Lakini tunaangalia pia ujenzi wa banda na malisho, inapaswa mfugaji avune mifugo yake anapoelekea wakati wa uhaba wa malisho na kuzingatia matibabu kwa mifugo yake sanjari na kuchukua mifugo ya miaka miwili hadi mitatu na aingize kwenye unenepeshaji kwa kipindi cha miezi mitatu ambao utafiti unaonesha kwa mfugo ambaye ana umri huo hajadumaa wanafanya vizuri,” amesema.
Kwa upande wake mfugaji kutoka Kata ya Mikinguni wilayani humo ambaye amehudhuria mafunzo hayo, Mbega Layani, ameishukuru serikali kupitia Bodi ya Nyama kwa kuwapa elimu juu ya ufugaji bora na unenepesha wa mifugo kwa muda mfupi kwani elimu hiyo itawasaidia kutoka kwenye ufugaji wa zamani na kufanya ufugaji wa kisasa wenye tija ili kupata mafanikio kwenye ufugaji wao.