Gavana wa zamani wa Lagos, Bola Ahmed Tinubu,ataapishwa leo kuwa rais mpya wa Nigeria.
Hii inafuatia uchaguzi uliokumbwa na utata mwezi Februari ambao unapingwa na upinzani mahakamani.
Huu ndio wakati Bola Ahmed Tinubu amekuwa akiusubiri katika kipindi chake chote cha kazi. Hatimaye ataapishwa kama kiongozi wa uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.
Lakini Bw Tinubu anarithi nchi yenye ukosefu mkubwa wa usalama,uchumi unaoyumba na wapiga kura waliogawanyika.
Rais anayeondoka madarakani Muhammadu Buhari ametetea miaka minane ya uongozi wake.
Katika hotuba yake ya mwisho kwa taifa siku ya Jumapili, Buhari alitetea rekodi yake ofisini baada ya majukumu mawili.
“Ninahisi kuridhika kwamba tumeanza kuzaliwa upya kwa Nigeria kwa kuchukua hatua muhimu za awali na nina hakika kuwa utawala unaokuja utaharakisha kasi ya kazi hii kuona Nigeria ambayo inatimiza hatima yake ya kuwa taifa kubwa” (…) “Nina imani kwamba ninaondoka madarakani na Nigeria bora zaidi mwaka 2023 kuliko 2015”, alihitimisha Muhammadu Buhari, rais anayemaliza muda wake wa Nigeria.
Rais mpya, Bola Tinubu, anatazamiwa kuapishwa siku ya Jumatatu huku nchi ikikabiliwa na matatizo ya kiuchumi na hali mbaya ya usalama.