Brazil itaadhimisha siku ya kitaifa ya ‘Siku ya Mfalme Pele’ mnamo Novemba 19 kila mwaka, kuadhimisha tarehe ambayo nguli huyo wa soka alifunga bao aliloliona kuwa la 1,000 katika maisha yake ya soka mwaka 1969.
Chapisho rasmi la serikali ya Brazil lilisema Jumanne kwamba Rais Luiz Inacio Lula da Silva alipitisha sheria inayoidhinisha heshima ya kitaifa kwa mshindi huyo mara tatu wa Kombe la Dunia.
Nyota huyo wa soka wa Brazil alifariki Desemba 29, 2022 akiwa na umri wa miaka 82.
Tarehe iliyochaguliwa kwa ajili ya sherehe hizo ni marejeleo ya siku ambayo Pele alifunga bao la ushindi la Santos kwa mkwaju wa penalti katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Vasco da Gama kwenye Uwanja wa Maracana mnamo 1969 – ingawa baadhi ya wanahistoria wa soka wanahoji kama hiyo ilikuwa mechi ya 1,000.