Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa kwa miaka yote wananchi wa Wilaya ya Bukombe wamekuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kiu ya maendeleo.
Amesema wananchi hao wana haki ya kuchagua kati ya maneno au maendeleo na wamekuwa wakitamani maendeleo kwa kuwa na shule, barabara na zahanati.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba 21, 2024 wakati akifungua Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Wilaya ya Bukombe zilizofanyika katika Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe Mkoa wa Geita.
“ Tunapozindua kampeni zetu tuna wajibu wa kuchagua maneno au maendeleo, tutashindanisha vyama kwa sera na kuonesha tuliyofanya kwa kipindi kilichopita. Tumekuja leo kuwaambia sisi tuko upande wa maendeleo na wengine wako upande wa maneno kama mwakilishi wenu nimekuja kuwaambia tuchague maendeleo, tuchague CCM,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “ Tuliwahi kupata viongozi wa chama kingine na sasa tuna wajibu wa kupima kati yao na CCM mabadiliko yako chama gani,”
Akielezea hali ya uandikishaji wapiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mtaa, amesema kuwa mwaka 2024 Bukombe imefanikiwa kuandikisha idadi kubwa ya wapiga kura ambayo ni 228,659 ikiwa ni rekodi ya juu katika mkoa na ukanda huo hali inayodhihirisha ushindi kwa CCM na hasa kutokana na utekelezaji wa ilani yake.
Halikadhalika, Dkt. Biteko amesema asilimia 70 ya vitongoji vina wagombea wa CCM huku vyama vingine vikishindwa kuweka wagombea.
“ Novemba 27, 2024 wote tukapige kura tunatakiwa kumshukuru Rais Samia kwa upendo na kwa kufanya jitihada nyingi za kutujengea barabara, shule za msingi na sekondari, vyuo vya VETA, shule ya amali na mengineyo kwa haya yote twende tukawapigie kura wagombea wa CCM,” amesema Dkt. Biteko.
Pamoja na hayo amewaasa wananchi wa Bukombe kuhubiri umoja, amani na upendo hata baada ya uchaguzi kuisha sambamba na wagombea hao kuhudumia wananchi wa Bukombe.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila amesema kuwa kazi ya CCM katika uchaguzi ni kushinda kwa ngazi zote za kata, vijiji, vitongozi.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Alexandrina Katabi amewataka wanachama wa CCM Wilaya ya Bukombe kuendelea kuimarisha umoja na ushirikiano wao hasa wakati huu wa kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Diwani wa Kata ya Bugelenga, Leonard Lubigisa akizungumza kwa niaba ya madiwani amewataka wanachama wa CCM kupiga kura ifakapo Novemba 27, 2024.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kupelekea maendeleo katika Jimbo hilo na kuhamasisha wananchi kuichagua CCM kwa jitihada zake za ujenzi wa barabara pamoja na miradi mingine.