Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania May 28, 2021 lilipitisha bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyolenga kutekeleza vipaumbele 13 kwa sekta zote mbili za Mifugo na Uvuvi.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kuhitimishwa kwa mjadala wa bajeti ya Wizara hiyo ambapo baadhi ya wabunge walitaka kupata ufafanuzi wa baadhi ya masuala yanayohusu sekta hizo mbili ikiwa ni pamoja na kutaka kujua namna Wizara hiyo ilivyojipanga kuendelea kushughulikia changamoto za wafugaji na wavuvi.
Akizungumza wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara hiyo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai mbali na kuishauri Serikali kuibinafsisha kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ili kuongeza ufanisi zaidi, aliwapongeza viongozi na watendaji wa Wizara hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuimarisha sekta za Mifugo na Uvuvi nchini.
“Kuongoza na kuiendesha Wizara hii sio rahisi kwa sababu inashughulikia kundi kubwa sana la Wananchi na ni miongoni mwa Wizara iliyozalisha ajira nyingi zaidi na ndio maana kutokana na umuhimu wake niliona ni vizuri tuijadili kwa mapana zaidi” Ndugai.
Ndugai alisema kuwa Bunge lake limekubali kupitisha kiasi chote cha fedha kilichoombwa na Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa sababu linaamini kuwa kama Serikali ikifanya uwekezaji kwenye Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi changamoto ya ukosefu wa ajira kwa Watanzania itapungua kwa kiasi kikubwa na hatimaye kumalizika kabisa.
Awali akianisha maeneo ya kipaumbele ambayo Wizara yake imejipanga kutekeleza kwa mwaka ujao wa fedha kwa upande wa Sekta ya Mifugo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema kuwa Wizara yake imejipanga kuboresha na kutafuta masoko ya mifugo na mazao yake, kuboresha kosaafu za mifugo,kuboresha malisho na upatikanaji wa maji na vyakula vya mifugo.
“Spika Wizara yetu pia kwa mwaka wa fedha ujao imedhamiria kuendelea kuimarisha afya ya mifugo, kuwezesha utafiti na mafunzo ya ugani na kutekeleza mpango wa kopa ng’ombe lipa ng’ombe na kopa mbuzi lipa mbuzi” Ndaki.
Akianisha maeneo ya vipaumbele ambayo Wizara yake imejipanga kuyatekeleza kwa upande wa sekta ya Uvuvi, Ndaki alisema kuwa kwa mwaka ujao wa fedha Wizara imejipanga kujenga bandari ya uvuvi na kununua meli tatu za uvuvi, kuimarisha mialo, masoko, vichanja vya kukaushia samaki, maghala ya ubaridi na mitambo ya barafu, kuweka mazingira wezeshi kwenye uvuvi wa bahari kuu na kuanzisha mashamba darasa ya ufugaji samaki katika Halmashauri 40 kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI.
“Spika kwa upande wa sekta ya Uvuvi pia tunakusudia kuongeza uzalishaji wa vifaranga na chakula cha samaki, kuimarisha ulinzi shirikishi na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi nchini na kuweka mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya utambuzi wa maeneo ya mavuvi” Ndaki.
Bunge limepitisha jumla ya shilingi Bil. 47. 8 zilizoombwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa upande wa sekta ya Mifugo na shilingi Bil. 121. 4 ambazo zitatumika kwa upande wa sekta ya Uvuvi kwa mwaka ujao wa fedha 2021/2022.