Katika muendelezo wa shughuli za maadhimisho ya miaka 10 ya CRDB ya Burundi , ujumbe wa Benki ya CRDB ulioongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Abdulmajid Nsekela aliyeambatana na wajumbe wa Bodi ya kampuni Mama ya Benki ya CRDB pamoja na kampuni tanzu ya Benki ya CRDB Burundi umetembelea Benki Kuu ya Burundi kutoa shukrani kwa ushirikiano mkubwa kwa Benki ya CRDB Burundi.
Akizungumza katika mkutano, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Burundi, Desire Musharitse alisema Benki Kuu ya nchi hiyo inafurahia sana kwa uwepo wa Benki ya CRDB nchini Burundi kwani imekua sehemu ya uwezeshaji wa miradi mingi ya kiuchumi kwa nchi lakini pia imechangia uwezeshaji wa wafanyabiashara.
“Tulipata matatizo yaliyopelekea changamoto kubwa ya upatikanaji wa fedha za kigeni mwaka 2015 lakini tulipata msaada mkubwa sana kutoka Benki ya CRDB na hakika hilo limedhihirisha ule usemi wa rafiki wa kweli hujulikana wakati wa shida” alisema Musharitse.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema Benki ya CRDB inatarajia kuingia nchini DRC hivi karibuni jambo ambalo litachangia kukuza biashara kati ya Burundi na DRC lakini pia ushirikiano wa biashara kati ya nchi hizo na Tanzania ambazo kwa pamoja ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Adhma yetu katika masoko tunayohudumia ni sio tu kutoa huduma bora bali kutoa mchango katika uchumi na kubadilisha maisha ya watu tunaowahudumia hivyo tunaahidi kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na Benki Kuu ya Burundi ili kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini Burundi” aliongeza Nsekela.