Mamlaka ya Majisafi na usafi wa mazingira Bukoba (BUWASA) imekabidhi site kwa mkandarasi ikiwa ni kiashiria cha kuanza rasmi kazi ya uboreshaji wa miundombinu ya maji katika manispaa ya Bukoba.
Tukio hilo limefanyika katika ofisi za Buwasa likiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Bukoba Mhandisi John Sirati huku likishuhudiwa na watumishi mbalimbali wa mamlaka hiyo sambamba na baadhi ya watendaji wa kata za manispaa ya Bukoba ambapo mradi huo utapita.
Akisoma taarifa ya mradi huo mhandisi Daudi Beyanga ambaye ni Meneja wa mradi huo amesema kuwa mradi unagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 1.3 na unatekelezwa na Mkandarasi Edonas Investment Limited Jv Rek One Co.Limited huku ukitarajia kukamilika ndani ya miezi sita.
Aidha amesema kuwa miongoni mwa kazi zitakazofanyika ni pamoja na kubadirisha mita za wateja 5000 ambazo zimekaa muda mrefu site na hazifanyi kazi vizuri,kuhamisha wateja waliopo kwenye bomba za chuma na kwenda kwenye bomba za UPVC,kugawa zone ya mjini katika zone ndogo saba na baada ya mradi kukamilika utanufaisha wananchi 8500 wa kata Bilele,Miembeni,Hamugembe na Bakoba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa BUWASA Mhandisi John Sirati amesema kuwa mradi huu ni wa muhimu sana kwani utatatua changamoto kubwa ya upotevu wa maji katika kanda ya mjini ambayo kwa sasa yanayopotea ni wasitani wa asilimua 35.6 huku akimtaka mkandarasi kuweka jitihada kubwa ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa.