Shirikisho la soka Afrika (CAF) limetangaza kuwa na mpango wa kutembelea viwanja vyote vitakavyotumika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
CAF wanataka kukagua viwanja hivyo sababu ya kutaka teknolojia ya usaidizi wa picha za video kwa waamuzi (VAR) kwa mwaka huu ianze kutumika kuanzia robo fainali na sio fainali pekee kama ilivyokuwa mwaka jana.
Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam Tanzania ni miongoni mwa viwanja vitakavyotumika kwani Simba SC imefuzu katika hatua hiyo.
Droo ya kupanga ratiba ya mechi za robo fainali itachezeshwa Ijumaa ya April 30 2021 ambapo timu zilizofuzu ni Simba SC, Mamelod Sundowns, Al Ahly, Wydad, Esperance, Kaizer Chiefs, MC Alger na CR Belouizdad.