Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limesema limewasiliana na mamlaka za Libya na Nigeria baada ya kujulishwa kwamba Timu ya Taifa ya Nigeria na benchi lake la ufundi walikwama katika uwanja wa ndege waliotakiwa kutuwa kwa saa 15.
CAF imesema sakata hilo limewasilishwa kwa Bodi ya Nidhamu ya CAF kwa ajili ya uchunguzi na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya wale waliokiuka Kanuni na Taratibu za CAF.
Hapo awali timu ya taifa ya Nigeria maarufu Super Eagles ilisusia kucheza mechi ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika, ikitaja kutelekezwa na kucheleweshwa katika uwanja wa ndege nchini Libya, siku ya Jumatatu.
Wachezaji na wafanyakazi wa Super Eagles walisafiri kwa ndege hadi Libya Jumapili usiku lakini wakaelekezwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Al Abraq badala ya kituo chao cha awali walichokusidia cha Uwanja wa Ndege wa Benghazi, ambao uko umbali wa zaidi ya kilomita 200 (maili 124) na saa tatu na nusu kutoka hoteli yao.
Baadhi ya wachezaji walidai waliachwa bila chakula na maji.
Mshambulizi wa Nigeria Victor Boniface alilalamika kuwa alikuwa amekwama kwenye uwanja wa ndege kwa takriban saa 13 bila chakula, mtandao wa intaneti (WiFi) wala mahali pa kulala. “Afrika, tunaweza kufanya vizuri zaidi,” alisema kwenye mtandao wa X.
“Kama kapteni, pamoja na timu, tumeamua kwamba hatutacheza mchezo huu,” William Troost-Ekong alisema kwenye mtandao wa X.
Shirikisho la Soka la Nigeria lilisema kwamba wakati ndege ya kukodi ya timu hiyo ilipokuwa ikishuka kuelekea Benghazi, ilielekezwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Al Abraq bila usafiri mbadala.