Cape Verde imekuwa nchi ya tatu ya kutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria barani Afrika, kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani WHO.
Hatua hii ya kisiwa cha Cape Verde chenye watu 500,000, kinaungana na Mauritius iliyotokomeza Malaria mwaka 1973 na Algeria mwaka 2019.
Kwa mujibu wa Shirika la afya duniani WHO, ili nchi kuwa huru dhidi ya ugonjwa huo ambao umeendelea kuwauwa maelfu ya watu barani Afrika hasa watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano, inapaswa kutoripoti kisa chochote cha maambukizi hayo kwa miaka mitatu mfululilizo.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameipongeza Cape Verde kwa kuushinda ugonjwa huo kutokana na mikakate yake ya kuimarisha sekta ya afya na ni mfano kwa mataifa mengine ya Afrika.
Duniani, ni mataifa 43 tu, ndio yaliyofanikiwa kuumaliza ugonjwa huo ambao mwaka 2022 pekee, ulisababsiha vifo vya watu 608,000 na kuwaambukiza watu wengine Milioni 250.