CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu wa Halmashauri Kuu(NEC) Itikadi, Uenezi, Siasa na Mafunzo CPA Amoss Makalla amesema Chama hicho katika kipindi chote Cha kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kitaheshimu ratiba ya mikutano sambamba na kufanya kampeni za kistaarabu na hakitamkejeli mtu yeyote.
CPA Makala ameyasema hayo leo Novemba 22,2024 katika Jimbo la Segerea mkoani Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
“Ahadi ya CCM katika kampeni hizi tutafanya kampeni za kistaarabu na tutatumia 4R za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan zinazohimiza kuheshimiana na kuvumiliana.CCM kama Chama kiongozi tutafanya kampeni za kistaarabu lakini tutaheshimu ratiba zote kama zilivyowekwa.Kote nchini Wana CCM tuheshimu ratiba na tuwe mfano.”
Pia amesema CCM haitatumia ukubwa wake kama Chama kiongozi kuvuruga ratiba bali watakuwa mstari wa mbele kuheshimu utaratibu wote uliowekwa kufanikisha kampeni hizo huku akitoa mfano mkoani Songwe kuna chama cha upinzani kimekurupuka na kwenda kufanya mkutano wakati ratiba haikuwa ya kwao,hivyo CCM haitakuwa tayari kuvamia mikutano ,wataheshimu ratiba.