Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe kimewataka wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji waliochaguliwa kwenda kusimamia shughuli za maendeleo na miradi inayoendelea kwenye maeneo yao kwa kufuata utaratibu,sheria na kanuni zilipo ili kufanikisha maendeleo kwenye jamii zao kuliko kutumia nafasi walizopata kujinufaisha na kuwanyanyasa wananchi.
Agizo hilo limetolewa na katibu wa Siasa na Uenezi mkoa wa Njombe Josaya Luoga wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake baada ya mchakato wa uchaguzi kukamilika ambapo amesema Chama hicho hakitoi maelekezo kwa wenyeviti kwenda kutoza fedha kwa ajili ya mhuri kwa wananchi badala yake wakatoe huduma huku akitoa tahadhari kuwa wasidhani wanakwenda kupata fedha kwa kuwa kazi hiyo ni ya kujitolea.
“Kazi ya uenyekiti wa kijiji,kitongoji au mtaa ni ya kujitolea sasa isiende kutumika kama ndio kazi mama kwa hiyo tunawaomba wakatumie nafasi zao vizuri kutatua kero za wananchi badala ya kutumia nafasi hizo kuwaumiza wananchi na kujipatia vipato visivyo halali kwa kuwa kwa utaratibu wetu unapoomba nafasi yoyote ndani ya Chama chetu ambayo ni ya kujitolea ni lazima ueleze kazi yako mama,sisi tunaamini tumepata viongozi wenye sifa ya kuwatumikia wananchi”amesema Luoga
Amesema katika uchaguzi uliofanyika Novemba 27 Chama hicho mkoa wa Njombe kimepata ushindi wa zaidi ya asilimia 99.7% ambapo katika vijiji 381 vya mkoa huo CCM imepata ushidi kwa kushinda vijiji 377 na katika mitaa 82 Chama hicho kimeshinda mitaa 81 na katika vitongoji 1832 wameweza kupata ushindi katika vitongoji 1819 huku kati ya wajumbe 3710 wakifanikiwa kupata 3698 ambapo amewashukuru wananchi na wanachama kwa kujenga imani kwa Chama hicho.