Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Shaka Hamdu Shaka ameonesha kukerwa kwake na tabia ya Fedha ya miradi ya Maendeleo kucheleweshwa kwa kisingizio cha Urasimu wa Mifumo ya Ulipaji kutofunguka kwa muda mrefu jambo ambalo linakwamisha baadhi ya Miradi utekelezaji wake kuenda kwa kasi na haraka kama inavyopangwa.
Hiyo ni baada ya kuelezwa kuwa kuna mradi wa maji kijiji cha Mwongozo Wilaya ya Kaliua Mkoa wa Tabora, umechelewa kutokana na mfumo wa ulipaji kuwa na matatizo ambapo kwa zaidi ya miezi mitatu wameshindwa kufanya malipo kwa kisingizio cha mfumo kutofunguliwa.
Shaka amesema haiwezekani mfumo huo kutofanya kazi kwa zaidi mwezi mzima jambo ambalo amesema inatumika kama kichaka cha kuficha uzembe wa baadhi ya watendaji wasimamizi na wakandarasi watekelezaji huku Wananchi wakisubiria huduma hizo za kijamii kwa muda mrefu.
“Mimi siamini..tutafuatilia kujua kama kweli mfumo huo umeshindwa kufanyakazi kwa zaidi ya mwezi mzima, Rais Samia anapotoa fedha za miradi alishasema anataka kuona fedha zinatumika katika muda husika, tusikwamishe miradi kwa kisingizi za urasimu katika mifumo, hili tutalishughulikia kwa ukaribu” alisema Shaka