CEO Rounda Table (CEOrt) na Chama cha Kimataifa cha Uhifadhi wa Asili na Maliasili (IUCN) vimetia saini makubaliano ya pamoja (MoU) yenye lengo la kuanzisha ushirikiano mkubwa unaolenga kukuza mbinu endelevu za biashara nchini Tanzania kwa kupambana na mabadiliko ya Tabia Nchi.
Chini ya Ajenda ya Kukuza Biashara Endelevu ya CEOrt na mkakati Endelevu na Ushirikishwaji wa IUCN kwa Maeneo ya Ukuaji Uchumi Barani Afrika (SUSTAIN), taasisi zote zitajikita katika kuboresha mazingira ya ndani ya biashara nchini Tanzania na kusaidia azma ya serikali katika kufikia malengo ya mabadiliko ya tabianchi ya kupunguza Viwango Vilivyowekwa Kitaifa (NDCs) kutoka 10-20% hadi 30-35% ifikapo mwaka 2030, ilielezwa Dar es Salaam wakati wa hafla ya kutia saini.
Santina Benson, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, alisema kwamba kutiwa saini kwa MoU hiyo ni sehemu ya ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili.
”Pia makubaliano haya yana lengo la kuiunga mkono Serikali katika kupunguza uzalishaji wa hewa isiyofaa kwa matumizi ya binadamu,” amesema.
“Tunashirikiana na wadau mbalimbali katika sekta binafsi kutekeleza malengo tofauti katika sekta za kiuchumi.
“Safari hii, tumekubaliana na Chama cha Kimataifa cha Uhifadhi wa Asili (IUCN) kufanya kazi pamoja na kuelimisha wadau katika biashara na uwekezaji kupitia sekta mbalimbali za biashara, ikiwa ni pamoja na kilimo, kuhusu fursa bora zilizopo kwa ukuaji wa biashara, ikiwemo upatikanaji wa mitaji kwa wakulima wadogo kupitia mabenki na taasisi nyingine za kifedha” alisema Benson.
“Ushirikiano huu pia utachangia katika maendeleo ya uchumi wa kijani jumuishi,” aliongeza.
Aliongeza zaidi, “Lengo la Maendeleo Endelevu (SDG) la 17 linasisitiza umuhimu wa ushirikiano ili kuleta matokeo chanya.
“ Ndio maana ushirikiano wetu na IUCN ulianza mwaka 2019 na tunafurahi kuwa na fursa ya kushirikiana tena na kuchangia kwa pamoja juhudi zetu za kukuza uchumi kwa kushirkiana na wadau mbalimbali,”
“Tunatambua jukumu muhimu la sekta binafsi katika kufikia malengo ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Tanzania,”
”Kupitia ushirikiano huu, tunajitolea kujenga msingi ambao utatoa elimu na kuonyesha fursa za biashara kwa wadau mbalimbali ili kusaidia biasharakukua,”
Ushirikiano huu unakuja wakati mwafaka baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hivi karibuni kuzindua Viwango vya Kimataifa vya Taarifa za Fedha (IFRS) ambavyo vitahitaji biashara zote kuweka mikakati ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
“Sekta binafsi ni mshirika muhimu katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza maendeleo chanya ya asili nchini Tanzania,”
”Kwa kutumia rasilimali zao, utaalamu, na mbinu za kulifika soko, taasisi za sekta binafsi zinaweza kuchangia kwa vitendo katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha uthabiti na kuchangia katika mfumo wa kuzalisha chakula endelevu.
Ushirikiano huu unalingana na jukumu la IUCN la kushirikiana na sekta binafsi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo uchafuzi wa mazingira.
”Kwa pamoja, tunakusudia kuchangia kikamilifu katika ajenda ya mazingira na tabianchi,” amesema Luther Anukur, Mkurugenzi wa Kikanda wa IUCN kwa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
CEOrt na IUCN watatumia utaalamu wao na rasilimali kutoa elimu kwa wadau juu ya ufanyaji mzuri wa biashara bila kuathiri mazingira
”Hii itafanikiwa kupitia vikao vya pamoja na wadau, utolewaji wa elimu, ili kuboresha utendaji mzuri wa biashara.