Chad siku ya Jumanne iliitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za kukabiliana na ugaidi katika eneo la Sahel, baada ya wanajihadi wa Boko Haram kuwaua takriban wanajeshi 40 wa Chad katika shambulio la kushtukiza.
Kundi la wanajihadi jana Jumapili lililenga ngome ya kijeshi katika eneo la Ziwa Chad, eneo linalokumbwa na makundi mbalimbali ya watu wenye silaha, katika shambulio lililosababisha vifo vya “askari 40 wa Chad”, serikali ilisema katika taarifa iliyochapishwa na msemaji Abderaman Koulamallah siku ya Jumanne. .
Takriban watu 20 pia walijeruhiwa, vyanzo vya kijeshi vilisema.
“Serikali inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzidisha uungaji mkono wake na kuimarisha usaidizi katika juhudi za kukabiliana na ugaidi hususan katika eneo la Sahel na bonde la Ziwa Chad,” ilisema taarifa hiyo.
“Hatua ya pamoja iliyodhamiriwa ni muhimu kutokomeza janga hili ambalo linatishia utulivu na maendeleo ya kanda nzima,” iliongeza.
Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby Itno Jumatatu alianzisha operesheni ya kuwasaka washambuliaji na “vikosi vya usalama kwa sasa vinawasaka washambuliaji”, taarifa hiyo pia ilisema.
Ubalozi wa Ufaransa nchini Chad ulisema katika chapisho la Facebook siku ya Jumanne kwamba “Ufaransa inasimama na Chad katika mapambano dhidi ya ugaidi” na kutoa rambirambi zake kwa mamlaka na familia za wanajeshi waliouawa.