Watanzania wameshauriwa kujenga tabia ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo karibu yao ili kuchochea maendeleo ya sekta ya utalii na kulinda rasilimali za taifa.
Wito huo umetolewa na baadhi ya wageni wa utalii kutoka Ujerumani waliotembelea mkoa wa Njombe kwa lengo la kujifunza kuhusu utalii wa kilimo cha chai.
“Sio mara yangu ya kwanza kuja Tanzania lakini ninaipenda sana hii nchi nimefanya kazi hapa lakini sikugundua kama kusini mwa Tanzania kuna mazingira mazuri,mkoa wa Njombe wanatakiwa wajivunie kwa mazao walionayo”amesema Werner Schurter mgeni kutoka Ujerumani
Kwa upande wao, wadau wa utalii wa mkoa wa Njombe wamesema ujio wa wageni wa kigeni ni ishara ya mafanikio katika juhudi za kukuza utalii wa ndani na kimataifa ambapo Michael Katona kutoka Kampuni ya Ramika Safaris and Tours pamoja na Michael Kalamu wameeleza kuwa mkoa huo una fursa kubwa za kitalii zinazoweza kuleta manufaa makubwa kiuchumi.
“Leo tumefanya utalii wa kilimo kwa kutembelea mashamba ya Chai Kibena na moja ya vitu walivyovutiwa wageni wetu ni pamoja na namna majani ya Chai yanavyopatikana kuanzia shambani mpaka kiwandani,kwa kweli tunaonaa furaha kuwa na sisi tunaweza kuhamasisha wenyeji na wageni kutembelea vivutio vyetu”amesema Katona
Baadhi ya wakazi wa Njombe wamesema ujio wa wageni wa nje unatoa fursa ya kutangaza mkoa kimataifa,huku ukileta fursa za kiuchumi kwa wenyeji.