Benki ya CRDB imesaini mkataba wa makubaliano na wachezaji Clatous Chama, Mohammed Hussein wa Simba SC pamoja na Aziz Ki na Farid Mussa wa Yanga SC kuwa mabalozi wake wa kufikisha elimu ya fedha kwa jamii kupitia kampeni yake ya “Benki ni SimBanking.” Mikataba na wachezaji hao imesainiwa katika makao makuu ya Benki ya CRDB na kushuhudiwa na viongozi waandamizi kutoka Benki ya CRDB pamoja na vilabu CEO wa Simba SC Imani Kajula na CEO wa Yanga Andre Mtine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela amesema Benki ya CRDB kwa muda mrefu imekuwa ikishiriki katika kusaidia jitihada mbalimbali za kimichezo kwa kutambua mbali ya kuwa michezo ni burudani, bali pia michezo ni biashara na uchumi pia.

Benki ya CRDB imefikia hatua ya kusaini makubaliano na wachezaji hao wa Simba na Yanga ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza wigo wa ufahamu wa elimu ya fedha kwa wachezaji wa soka na jamii kwa ujumla lakini pia ikiwa pia ni sehemu ya kutambua viwango vizuri ambavyo vimeonyeshwa na wachezaji hao katika kusaidia timu zao kupata matokeo mazuri lakini pia nidhamu ambayo wameonyesha katika mchezo jambo ambalo ni muhimu sana kwa mafanikio ya mchezaji.
