Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimeitaka serikali kujenga chumba cha kuhifadhi maiti katika Kituo cha Afya Maramba ili kuwapunguzia wananchi gharama za kusafirisha miili umbali mrefu hadi Hospitali ya Mkoa ya Bombo kwa ajili ya hifadhi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, MCC Rajabu Abdallah, akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa, alieleza kuwa chama hicho kimeamua kushirikiana na serikali kwa kuchangia mifuko 300 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa chumba hicho ambapo ni kuelekea maadhimisho ya miaka 48 kuzaliwa Kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Sisi kama chama tutachangia mifuko 300 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha kuhifadhi maiti, kwani hospitali hii tangu ilipojengwa mwaka 1973 haina chumba hicho. Hivyo basi, tunaiomba serikali kuanza ujenzi haraka ili kuwasaidia wananchi,” alisema Rajabu Abdallah.
Hatua hii inalenga kupunguza changamoto zinazowakumba wananchi wa Maramba, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya huduma hiyo muhimu.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mkinga Dkt. Salvio Samweli Wikesi ameseme kuwa huduma karibu zote zinatolewa na kuongeza kuwa “Kituo hiki ni Moja ya kituo kikubwa kwani kinahudumia wananchi elfu 46 na kinaona wagonjwa 70 kwa siku na tunatoa huduma ya upasuaji na wamama watano wanajifungua kwa siku”