Aliekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mgombea wa nafasi hiyo katika uchaguzi wa jana, Freeman Mbowe, amewasihi viongozi watakaoshika nyadhifa, wakijenge chama katika misingi ya maadili na nidhamu.
Akifugua mkutano wa chama hicho jana, Mbowe alisema: “Tumeona minyukano kadha wa kadha. Jambo hili si sifa, ni aibu ya chama ambayo hatupaswi kuliendeleza. Yeyote atakayechukua kijiti cha kukiongoza chama hiki, Kamati Kuu ijayo, wajibu wa kwanza tunaowaachia warithi wa mikoba yetu ni kurejesha nidhamu, kurejesha kuheshimu maadili ya chama hiki na kuhakikisha hakuna matusi ndani ya CHADEMA,” alisema.
Mbowe alisema wajibu wa viongozi wajao ni kuhakikisha kila mwana CHADEMA anamjenga mwenzake na kuimarisha chama kama taasisi.
“Ambaye atakataa kukubaliana na msimamo huu, huyo si mwenzetu. Niwashauri na kuwasihi sana, uwapo wetu leo unaakisi maumivu na jasho la watu walioumia kuijenga CHADEMA,” alisema.
Alisema minyukano, kubezana na kudhalilishana haupaswi kuwa utamaduni wa CHADEMA kwa kuwa inabomoa haiba na heshima ya chama, hivyo kusisitiza kuwa wanachama, viongozi na wafuasi wa CHADEMA wana dhamana ya kukilinda chama kwa gharama yoyote.
“Chama hiki hatutakiruhusu kwa namna yoyote eti kwa sababu pengine kura za Mbowe, Lissu au Odero hazikutosha, uchaguzi huu haupaswi kuwa vita bali unapaswa kuwa furaha ya ujenzi wa demokrasia,” alisema.