Zaidi ya chanjo milioni moja za polio zilizokusudiwa kutolewa kwa watoto zimeharibiwa ikiwa ni matokeo ya uporaji nchini Sudan. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF lilisema siku ya Ijumaa.
Uharibifu huo umetokea huku mzozo ukiendelea kati ya jeshi la Sudan na vikosi Rapid Support Forces uliozuka mwezi Aprili.
Naibu mkurugenzi wa Ofisi ya Mipango ya Dharura katika UNICEF, Hazel De Wet alisema vifaa kadhaa baridi vya kuhifadhi chanjo vimeporwa, kuharibiwa na kuangamizwa huko Darfur Kusini.
Shirika hilo lilikuwa katikati ya kampeni mfululizo za utoaji chanjo ya polio nchini Sudan. Kampeni ambazo zilifuatia mlipuko wa ugonjwa huo mwishoni mwa mwaka 2022.
UNICEF ni miongoni mwa mashirika kadhaa ya misaada ya kibinadamu yaliyoripoti uporaji wakati wa mzozo wa Sudan.