Katika mkutano uliofanyika huko Beijing China, Tanzania, na Zambia zimetia saini makubaliano ya awali kuhusu mradi wa reli ya Tanzania-Zambia ambao unalenga kuboresha mtandao wa usafiri wa reli na bahari katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Rais wa China, Xi Jinping alishuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo ya reli ya Tanzania-Zambia pamoja na marais wa Tanzania na Zambia, waliokuwa Beijing kuhudhuria Mkutano wa Ushirikiano wa China na Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa ya kituo cha televisheni cha CCTV, Rais Jinping alisema, “China iko tayari kuchukua mkutano huu kama fursa ya kuleta maendeleo mapya katika kuufufua mradi wa reli ya Tanzania-Zambia, kushirikiana kuboresha mtandao wa usafiri wa reli na bahari katika Afrika Mashariki, na kuijenga Tanzania kuwa eneo la mfano kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa hali ya juu kati ya China na Afrika.”
Aidha mapema mwaka huu, Benki ya Dunia iliidhinisha ufadhili wa dola milioni 270 kusaidia kuboresha usafiri kati ya Tanzania na Zambia na kuimarisha biashara ya kikanda. Njia ya Dar es Salaam kati ya nchi hizo mbili, ambayo ni muhimu kwa usafirishaji wa shaba kutoka eneo la Copperbelt katikati ya Afrika, inahudumiwa na Mamlaka ya Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA).