Mamlaka za China zimewaua kisheria wafungwa wawili waliohukumiwa kifo miezi miwili baada ya kutekeleza mashambulizi ya gari na kisu yaliyosababisha vifo.
Shirika la habari la serikali ya China la Xinhua linasema mwanamume mwenye umri wa miaka ya 60 aliyegomga umati kwa gari na kuua watu 35 aliuawa jana Jumatatu.
Shambulizi hilo lilifanyika mwezi Novemba mwaka jana kwenye kituo cha michezo katika mji wa Zhuhai jimboni Guangdong. Alihukumiwa kifo kwa kuhatarisha usalama wa umma.
Mwezi huo huo, mwanamume aliyekuwa na kisu mwenye umri wa miaka ya 20 alifanya shambulizi kwenye shule ya mafunzo ya kiufundi katika mji wa Wuxi jimboni Jiangsu na kuua watu wanane na kuwajeruhi wengine 17. Alihukumiwa kifo na pia aliuawa jana Jumatatu.
Mashambulizi hayo ya kiholela dhidi ya raia yaliyosababisha vifo na majeraha yanasemekana kuakisi kutoridhishwa kwa watu katika uchumi na jamii ya China.
Baada ya tukio la Zhuhai, Rais wa China Xi Jinping aliziagiza mamlaka kuwaadhibu vikali wahusika na kufanya juhudi zao kubwa kudumisha uthabiti katika jamii.
Kwa kuwaua wanaume hao haraka baada ya matukio hayo, mamlaka za China zinaonekana kutaka kuonyesha azimio lao la kuzuia uhalifu kama huo.