Raia wa China, Yang Feng Glan ‘Malkia wa Tembo’ ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kauli ya Rais John Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’ haitekelezwi mahakamani kwa sababu ushahidi kesi yake unaahirishwa mara kwa mara.
Mbali ya Feng, wengine ni Salvius Matembo na Philemon Manase ambapo wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi wakidaiwa kufanya biashara ya vipande 706 vya meno ya Tembo vyenye uzito wa kilogramu 1889 zenye thamani ya Sh.bilioni 13.
Feng alitoa kauli hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, baada ya wakili wa Serikali, Wankyo Simon kudai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Wakili Simon aliieleza mahakama kuwa walitarajia kuwa na shahidi lakini anaumwa, hali yake bado siyo nzuri.
Baada ya kueleza hayo, Feng amedai kuwa anakumbuka Jaji Mkuu alisema kesi zote za zamani zimalizike kwa haraka, lakini kesi yake imekuwa ikipangiwa kusikilizwa mfululizo huku mashahidi wakishindwa kufika.
“Pia hata Rais John Magufuli anasema Hapa Kazi Tu, nikasema sasa mbona mahakama haina hapa kazi tu, nipo mahabusu naumwa moyo, misuli inauma, kidole kimekufa ganzi, lakini najitahidi nakuja”.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Shaidi aliutaka upande wa mashtaka upeleke mashahidi.
Kesi hiyo imeahirishwa na itaanza kusikilizwa mfululizo kuanzia November 21,24,27,28,29,30 na December 1, 2017.
Ulipitwa na hii? Shahidi kesi ya Malkia meno ya Tembo hajatokea Mahakamani