Serikali nchini Congo-Brazzaville imetupilia mbali ripoti za kuwepo kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya utawala wa rais Denis Nguesso, ambaye amekuwa akitawala kwa kipindi cha miaka 39.
Matamshi ya serikali yanakuja baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba jeshi lilikuwa linajaribu kuangusha utawala wa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 79 anayehudhuria mkutano wa awamu ya 78 wa umoja wa mataifa jijini New York.
Kupitia ujumbe kwenye ukurasa wa X zamani ukijuliakana kama twitter, waziri wa mawasiliano kwenye taifa hilo Thierry Moungalla amesema taarifa hizo ni za uongo.
Waziri huyo amewahakikisha raia wa Congo kuwa nchi yao iko salama na hakuna hofu yoyote ya kutoendelea na shughuli zao za kila siku.
Wito kama huo pia ulichapishwa kwenye wavuti wa serikali, ukitaja ripoti hizo za mapinduzi kama zisizokuwa za kweli.
Rais Nguesso aliingia madarakani katika taifa hilo lenye utajiri wa mafuta kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 1979.
Kiongozi huyo wa Congo, ndiye rais wa tatu ambaye amekuwa madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika baada ya mwenzake wa Equatorial Guinea Teodoro Obiang na yule wa Cameroon Paul Biya.