Jamhuri ya Kongo imetangaza janga la homa ya MPOX, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya monkeypox, baada ya kesi 19 kuthibitishwa katika mikoa mitano, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Brazzaville.
Ripoti iliyotolewa na Reuters jana Jumatano ilimnukuu Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Congo, Gilbert Mokoki, akisema hakuna vifo vilivyorekodiwa lakini ametoa wito kwa umma kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kuepuka kuwasiliana kwa karibu watu wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo, kuepuka kukaribia wanyama na kuepuka kushika nyama bila glovu za mikono
Ikumbukwe kuwa mwaka 2022, baada ya mfululizo wa mashauriano na wataalamu wa kimataifa, hatimaye shirika la Afya la Afya Duniani ( WHO) lilianza kutumia jina MPOX badala ya Monkeypox au Homa ya Ndui na Homa ya Nyani kwa maelezo ya kwamba lilikuwa linasababisha mambo kadhaa ikiwemo unyanyapaa.
MPOX iligunduliwa kwa mara ya kwanza kwa binadamu katika nchi jirani ya DR Congo mwaka 1970, kulingana na WHO.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani, tangu mwanzoni mwa Mei 2022, visa vya ugonjwa wa MPOX vimeripotiwa katika nchi ambazo ugonjwa huo si wa kawaida na unaendelea kuenea katika nchi kadhaa.
Mlipuko mkubwa wa kwanza wa maambukizi ya binadamu kwenda kwa binadamu, ambao ulikuwa mwaka 2017 nchini Nigeria, ulisababisha zaidi ya visa 200 vilivyothibitishwa. Hivi karibuni, jarida la Nature limechapisha ripoti isemayo kuwa ugonjwa huo unaweza kueneza kupitia uhusiano wa kingono.