Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali watu CP Suzan Kaganda amewataka Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto kote nchini kutoa elimu zaidi ili kumaliza vitendo vya ukatili katika Jamii huku akiwapongeza Watendaji wa dawati hilo kwa kufuatili kesi za ukali kwa karibu na wahusika kufikishwa mahakamani.
CP Kaganda ameyasema hayo leo Disemba 12, 2023 wakati wa mkutano na Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar unaoendelea Jijini Dodoma.
Ameongezea kuwa Jeshi la Polisi nchini litaendelea kuwatumia watalamu wa ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo mzuri watendaji wa dawati la jinsia na watoto.
Kwa Upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Maria Nzuki amesema kutokana na kazi nzuri ya kutoa elimu kwenye nyumba za ibada iliyofanyika siku ya Jumapili katika makanisa mbakimbali Jijini Dodoma tayari Makanisa zaidi ya 20 yameomba Watendaji wa dawati hilo kuwapatia Elimu ili kuwaongezea maarifa ya namna bora ya kutatua changamoto za ukatili wa kijinsia.
Pia amebainisha kuwa Madawati ya Jinsia na Watoto ambayo yapo chini ya Jeshi la Polisi yameendelea kuwa kimbilio katika kubaini na kuzuia Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia hapa nchini ambapo wananchi wengi wamezidi kuwa na uelewa mzuri zaidi juu ya vitendo vya ukatili.