Cristiano Ronaldo amekuwa mchezaji wa kwanza kwenye Ligi Kuu Hispania kufikisha mabao 25 kwa misimu mitano mfululizo.
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid na Ureno amekuwa moto kwa kutikisa nyavu tangu alipojiunga kwenye ligi hiyo ya Hispania akitokea Manchester United kwa ada ya Pauni 80 milioni mwaka 2009.
Bao pekee alilofunga mchezaji huyo dhidi ya Malaga Jumamosi iliyopita limeifanya Real Madrid kuzidi kujitanua kileleni huku mwenyewe akinogesha akaunti ya mabao na kufikisha 25 msimu huu.
Kwenye misimu mitano, Ronaldo amekuwa na rekodi nzuri ya kufunga kwenye ligi, msimu wa kwanza alifunga mabao 26, kabla ya misimu iliyofuata kufunga 40, 46, 34 na msimu huu hadi sasa ana mabao 25 na hivyo ana nafasi ya kuongeza mabao zaidi.
Kwa ujumla, Ronaldo amefunga mabao 240 katika mechi 235 alizoichezea Real Madrid.