Taasisi yetu ya CRDB Bank Foundation leo imezindua kambi ya mafunzo (boot camp) ya biashara changa za vijana 196 (startups) zilizoingia katika hatua ya mafunzo kabla ya kupewa mitaji wezeshi kwa ajili ya kuendeleza biashara zao.
Uzinduzi wa kambi hiyo umefanyika leo katika kituo maalum cha kuendeleza biashara changa kilichopo Makao Makuu ya zamani ya Benki ya CRDB yaliyopo mtaa wa Azikiwe jijini Dar es Salam na kuhudhuriwa na viongozi wa Benki, CRDB Bank Foundation, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), na Tume ya TEHAMA (ICTC).
Katika kambi hiyo biashara changa zitapewa mafunzo juu ya usimamizi wa uendeshaji wa biashara, utawala bora, matumizi ya mifumo ya kidijitali, vihatarishi na udhibiti wa biashara, na pamoja na fursa za uwekezaji katika masoko ya mitaji.