JESHI la Polisi Mkoa wa Mara limewakamata watu saba wakiwemo viongozi wawili wa Serikali ya kijiji cha Park Nyigoti, wilaya ya Serengeti baada ya kutuhumiwa kuwakamata na kuwafunga vitambaa usoni watu nane wanaowatuhumu kwa uchawi kisha kuwachapa viboko na kusababisha vifo vya watu watano.
Kaimu Kamanda wa Polisi na kamishina msaidizi wa Jeshi la Polisi ACP Ernest Kimola, amesema tukio hilo limesababisha watu wengine watatu kujeruhiwa kwa viboko na kulazwa katika Hospitali teule ya Nyerere DDH mjini Mugumu, mbali na mwenyekiti na mtendaji viongozi wawili wa jadi wamekamatwa wakihusishwa na mauaji hayo.
Wananchi hao walikamatwa katika miji yao kisha kufunga vitambaa usoni na kuchapwa viboko hadi kufa kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya ushirikina, viongozi hao wa jadi kwa kushirikiana na Serikali ya kijiji waliitisha mkutano kwa lengo la kuwabaini watu wanajihusisha na ushirikina ambao umesabisha mvua kutonyesha kijijini hapo ambapo watu wanane walitajwa katika mkutano huo.
Kaimu Kamanda huyo amewasema tukio hilo lililotokea alfajiri March 2 na kisha miili ya waliouawa ikitupwa karibu nyumba zao huku watu wengine watatu wakilazwa Hospitali kutokana na majeraha ya kupigwa.
CHANZO: Habari ITV March 05, 2015