Rapa staa wa Tanzania Roma Mkatoliki ambaye hivi karibuni aligonga headlines kwenye mitandao mbalimbali baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana na kupelekwa kusikojulikana pia amesema anaendelea vizuri baada ya mkasa huo.
Akizungumza kwenye interview ya Clouds 360 ya Clouds TV leo May 1, 2017 Roma amesema licha ya kutajwa sana katika harakati kutokana na aina ya muziki wake anaoufanya lakini hafungamani na chama chochote cha siasa.
“Naendelea vizuri, baadhi ya vidonda vimeanza kukauka. Mimi sifungamani na upande wowote, sina kadi ya chama chochote. Kwa sababu nikichukua kadi ya chama chako nakuwa familia yako, hata hivyo mimi ni Mkristo ‘Mkatoliki’, kwa hiyo katika hali ngumu huwa nasali kumuomba Mungu.
Mbali na kuelezea hali yake, pia Roma alisikitishwa na kitendo cha Mbunge wa Nkasi Ally Kessy ambaye alitaja jina lake Bungeni akidai aliimba wimbo kumhusu Rais na kusema alichokisema Mbunge huyo hakikuwa kweli.
“Tena alitaja kabisa jina langu. Lakini ameongea vile kwa sababu yeye ana mahali pa kusemea. Je, mimi nitasemea wapi? Hayo maneno bora angeongea Rais wa Manzese Madee ningejua swahiba wangu ananitania.
Aidha, kuhusu kazi Roma amesema kuwa sasa kazi zao zimekwama na wanashindwa kufanya vitu vingi kutokana na hasara kubwa iliyopatikana katika studio za Tongwe Records ambapo dua yao kubwa kwa sasa ni ajitokeze mtu au watu wanaoweza kuwasaidia kurejesha vifaa vilivyochukuliwa katika studio yao.
“Mimi ni msanii, mimi ni mfanyabishara. Hivyo lazima kazi ziendelee. Ndio maana hata sasa nimeona nitoke kuhangaika ili tuendelee. Kama tunaweza kusaidiwa, tunaomba mtu yeyote aweze kuona jambo la studio kwa jicho tofauti.” – Roma Mkatoliki.
VIDEO: Miaka 15 ya Q Chilla kwenye game ya Bongofleva