Daktari Bingwa wa Pua, Koo na Masikio, Dkt. Jane Bazilio wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi, Kibaha amewashauri Watu kutoingiza maji kwenye masikio yao wakati wa kuoga au kuyasafisha kwa kutumia pamba za masikio kwani kwa kawaida sikio hujisafisha lenyewe.
Dkt. Bazilio ameyasema haya wakati wa kambi ya huduma za kibingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete na kusisitiza kuwa sikio huwa linajisafisha lenyewe hivyo Mtu anapotumia pamba anakuwa anatoa nta iliyoko kwenye sikio ambayo kazi yake ni kulilinda sikio.
“Katika kambi hii tumewaona Wagonjwa wengi wenye matatizo ya masikio na pua, Wananchi wengi wanafikiri ile nta ni uchafu kutokana na rangi yake ile ya brown (kahawia) na kusema wanatoa uchafu ile sio uchafu ina kazi yake ya kulinda sikio, nta ile msiitoe ina utaratibu wake wa kutoka kwenye sikio”
Amesema Wagonjwa wengi waliojitokeza kwenye kambi hiyo wanakuwa na shida ya fangasi masikioni ambayo husababishwa na unyevunyevu kwenye masikio hivyo akawataka Watu wasiingize maji kwenye masikio yao pindi wanapooga au kunawa kichwa.
Daktari huyu amewashauri pia Wazazi na Walezi kuacha kuwasafisha Watoto wadogo kwa pamba kwani wanaposafisha nta ile inaweza kuingia kwenye sikio na kusababisha kuziba kwa sikio na kwamba ni hatari hata kwa Watu wazima pia.