Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo ACP Advera Bulimba amesema kuwa ofisi yake imejipanga kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya mbolea katika msimu ujao wa kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija ya mazao yanayolimwa wilayani humo.
ACP Bulimba ameyasema hayo leo wakati alipotembelewa ofiini kwake na Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ambao wako katika ziara ya kujifunza na kusikiliza changamoto za wadau katika Kanda ya Ziwa na Kati ili kuweza kuwa na namna bora ya kutatua changamoto hizo.
Sambamba na uhamasishaji wa mbolea ACP Bulimba amesema watahamasisha wafanyabiashara wa mbolea kuchangamkia fursa ya kufungua maduka ya mbolea na pembejeo katika wilaya hiyo ili huduma ya mbolea ya ruzuku inayotolewa na serikali iweze kuwafiki wakulima wote katika wilaya hiyo.
Amesema Wilaya ya Biharamulo ina misimu miwili ya kilimo na hivyo inahitaji kiasi kikubwa cha mbolea ili kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara.
Aliongeza kuwa kutokana na jiografia ya Wilaya hiyo kuwa na kata kuwa mbalimbali kuna haja ya kuwa na mawakala wengi zaidi ili kuwafikishia wakulima mbolea kwa wakati.
Akizungumza awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TFRA Dkt. Anthony Diallo alisema ni lazima Wilaya hiyo ijiwekee mikakati mahususi ya kuongeza matumizi ya mbolea kwa kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea ili kuongeza uzalishaji.
Dkt. Diallo alisema kuwa Wilaya ya Biharamlo ni miongoni mwa Wilaya yenye matumizi ya mbolea kidogo sana wakati ina eneo kubwa linalofaa kwa kilimo.
Alisema bila matumizi ya mbolea katika kilimo ni vigumu kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali na wenye tiija.
Mwenyekiti Diallo aliongeza kuwa mbolea ni biashara, hivyo Wilaya ijiwekee mikakati ya kuwavutia wafanyabiashara waje kuwekeza wilayani humo ili kuwasogezea wakulima huduma ya upatikanaji wa mbolea.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na uvuvi katika wilaya hiyo Dkt. Sospeter Mashamba amesema kuwa mahitaji ya mbolea katika wilaya hiyo ni tani 400 kwa mwaka ambapo hadi sasa wakulima zaidi ya 25,000 wameshasajiliwa kupata mbolea ya ruzuku ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
Dkt. Mashamba amesema Wilaya imeanza mikakati ya kushirikiana na kampuni ya mbolea ya minjingu ili kuanzisha mshamba darasa katika Wilaya hiyo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kutumia mbolea.