Ili kukuza kiwango cha taaluma kwa wanafunzi wa halmashauri ya mji wa Njombe,mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amekabidhi vitabu zaidi ya 8000 vya rejea kwa shule za sekondari 17 na shule binafsi 4 katika halmashauri hiyo vilivyotolewa na mbunge wa jimbo la Njombe mjini Deo Mwanyika.
DC Kissa amesema Rais Samia amewekeza kiasi kikubwa kwenye elimu ikiwemo ujenzi wa miundombinu nchi nzima hivyo jambo lililofanywa na mbunge wa jimbo hilo Deo Mwanyika ni katika kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais pamoja na kuchagiza kukuza viwango vya taaluma kwa wanafunzi.
“Hatuwezi kuacha kutambua jitihada ambazo zinafanywa na Mh Rais wetu Daktari Samia Suluhu Hassan katika kuboresha miundombinu ya elimu na sisi tunayonafasi ndogo ya kufanya na kila mtu akitimiza wajibu wake tutaweza kuivusha elimu yetu”amesema Kissa
Mbunge wa Njombe mjini Deo Mwanyika amesema miongoni mwa vitabu vya rejea vilivyokabidhiwa ni pamoja na vya masomo ya hesabu ,kemia,biolojia na fizikia hivyo ametoa wito kwa walimu na jamii kujenga utamaduni wa kusoma vitabu ili kuongeza maarifa na uelewa zaidi.